





























Hadeeth Cards
Da'wa cards that highlight great meanings from the noble prophetic hadiths in a simple style and attractive display that helps the Muslim to have a deeper understanding of his religion in an easy way
All
Kutoka kwa Abuu Masoud Uqba ni Amri Al-Answari Al-Badri radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu: "Hakika katika yale waliyoyakuta watu miongoni mwa maneno ya kiutume ya mwanzo, usipokuwa na haya basi fanya ulitakalo".
Imepokelewa na Al-BukhaariyAmeeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa katika yale yaliyokuja na usia ndani yake kutoka kwa Manabii waliotangulia, na yakaenea kwa watu na watu wakarithishana kutoka kwao karne baada ya karne, mpaka yakamfikia wa mwanzo katika umma huu, ni; tazama unayotaka kuyafanya, ikiwa yatakuwa ni katika mambo ambayo si aibu basi fanya, na ikiwa ni katika mambo ya aibu basi acha; kwa sababu kinachozuia kufanya matendo mabaya ni haya, atakayekosa aibu basi hutumbukia katika kila machafu na maovu.
Kutoka kwa Omari bin Khatwab radhi za Allah ziwe juu yake kutoka kwa Mtume rehema na amani za Allah ziwe juu yake alisema: "Laiti nyinyi mgetegemea kwa Mwenyezi Mungu ukweli wa kumtegemea, basi angekuruzukuni kama anavyowaruzuku ndege, wanatoka asubuhi wakiwa na njaa, wanarudi jioni wakiwa wameshiba".
Imepokelewa na Imam Ahmad, Tirmidhiy, Nasai, Ibn Majah na Ibn Hibban katika Sahih yake na HaakimAnatuhimiza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kuleta manufaa na kuzuia madhara katika mambo ya Dunia na Akhera, kwani hakuna yeyote mwenye kutoa wala kunyima wala kudhuru wala kunufaisha isipokuwa Yeye Aliyetakasika na Kutukuka, Na tufanye sababu zinazoleta manufaa na kuzuia madhara, pamoja na kumtegemea Mwenyezi Mungu kwa dhati, wakati wowote tutakapofanya hivyo, Mwenyezi Mungu ataturuzuku kama anavyowaruzuku ndege wanaotoka asubuhi wakiwa na njaa, kisha wanarudi jioni matumbo yakiwa yamejaa, na kitendo hiki kwa ndege ni aina ya kufanya sababu za kutafuta riziki, bila kubweteka wala uvivu.
Imepokelewa kutoka kwa Nawwaas bin Sam'aan Al-Answaariy -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- kutoka kwa Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- amesema: "Wema ni tabia njema, na dhambi ni lile lililokukereketa katika nafsi yako na ukawa hukupendezwa watu walione". Na kutoka kwa Wabiswa bin Ma'bad -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- Amesema: Nilimjia Mtume -rehema na amani ziwe juu yake-, Akasema: "Umekuja kuuliza kuhusu wema?" Nikasema: 'Ndiyo' Akasema: "Uchunguze moyo wako, Wema ni ule ambao nafsi itatulizana kwake, na moyo ukatulizana, na uovu ni ule unaokereketa ndani ya nafsi, na ukawa unatia shaka ndani ya kifua, hata kama watu watakupa majibu mazuri kiasi gani".
Hadithi ya kwanza ameipokea Muslim, na hadithi ya pili ameipokea Ahmad na Ad-DarimiAmeeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuhusu wema na uovu, akasema: Hakika jambo kubwa zaidi katika wema ni tabia njema pamoja na Mwenyezi Mungu kwa kumuogopa, na pamoja na viumbe kwa kustahamili maudhi yao, na kupunguza hasira, na kukunjua uso, na kuwa na maneno mazuri, na kuunga udugu na utiifu na upole na kuwapa watu udhuru na kuishi nao vizuri na ujamaa mzuri. Nakuwa wema ni ule uliotulizana kwao moyo na nafsi. Na ama dhambi ni katika lile ambalo nafsi itataharuki kutokana na mambo yenye utata na ikapata shaka pasina kukunjuka kifua, na moyo ukapatwa na shaka, na ukaogopa kwakuwa ni dhambi, ukawa haukutaka kulidhihirisha kwakuwa ni jambo baya kwa mtu na kwa watu wengine pia, na hii ni kwa sababu tabia ya nafsi hupenda kutazamwa na watu wengine ikifanya kheri; na hata kama watu watakupa majibu mazuri usichukue majibu yao madamu alama za utata zinazunguka ndani ya nafsi yako majibu yao hayawezi kuondoa utata madamu utata ni wa kweli na akawa anayekupa majibu anatoa pasina elimu; ama ikiwa majibu yanatokana na dalili ya kisheria kilichowajibu kwa mpewa majibu arejee katika hilo, hata kama moyo wake hautokunjuka kwa hilo.
Kutoka kwa Abdallah bin Busri radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema: Mtu mmoja alikuja kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake, akasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Hakika sheria za Uislamu zimekuwa nyingi kwetu, ni mlango gani tushikamane nao uliokusanya mambo mengi? Akasema: "Ulimi wako usiache kuwa mbichi kwa kumtaja Mwenyezi Mungu". Na katika riwaya nyingine: Miongoni mwa hadithi za Muadhi radhi za Mwneyezi Mungu ziwe juu yake: Maneno ya mwisho niliochana na Mtume rehema na amani ziwe juu yake nilisema: Ni amali ipi bora na iko karibu zaidi na Mwenyezi Mungu? Akasema: "Ni ufe hali yakuwa ulimi wako ni mbichi kwa kumtaja Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na Kutukuka".
Imepokelewa na Ahmad, Tirmidhiy, Ibn Majah na Ibn HibbanMtu mmoja alilalamika kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa ibada za sunna zimekuwa nyingi kwake mpaka zikamshinda kwa sababu ya udhaifu wake, kisha akamuuliza Mtume rehema na amani ziwe juu yake amuelekeze katika amali nyepesi itakayompa thawabu nyingi atakayoshikamana nayo na adumu nayo. Mtume rehema na amani ziwe juu yake akamuelekeza kuwa ulimi wake uwe mbichi utikisike kwa kudumu kumtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu kila wakati na kila hali; kama kumsabihi na kumhimidi na kumtaka msamaha na kumuomba na mfano wake.
Imepokewa kutoka kwa Abuu Bakra -Radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: amesema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-: "Hivi nikuelezeni madhambi makubwa?" Kalisema hilo mara tatu, wakasema: Tueleze ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, akasema: "Ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu (na kitu kingine), na kuwaasi wazazi wawili" Na akakaa vizuri na alikuwa kaegemea, akasema: "Fahamuni, na kusema uongo", akasema: Akaendelea kulikariri neno hilo mpaka tukasema: Laiti angenyamaza.
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeAnawaeleza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- Masahaba zake kuhusu madhambi makubwa, akataja haya matatu: 1- Ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu: Nako ni kuielekeza aina yoyote katika aina za ibada kwa asiye Allah, na kumfanya kuwa sawa na Allah asiyekuwa Allah katika uungu wake na uumbaji na ulezi wake na majina yake na sifa zake. 2- Kuwaasi wazazi wawili: Nayo ni kila aina ya maudhi kwa wazazi wawili, sawa sawa iwe kwa kauli au kitendo, na kuacha kuwafanyia wema. 3- Kauli ya uongo ikiwemo ushahidi wa uongo: Nayo ni kila kauli ya kuzusha ya uongo, yenye lengo la kumdhalilisha yule anayekusudiwa kwa kuchukua mali yake au kumfanyia uadui katika heshima yake au mfano wa hayo. Alikariri Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- tahadhari hii ya kusema uongo ikiwa ni tahadhari juu ya ubaya wake na athari zake mbaya kwa jamii, mpaka wakasema Masahaba: Laiti angelinyamaza; Kwa sababu ya kumhurumia, na kwa kuchukia kile kinachompa kero Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-.
Imepokelewa Kutoka kwa Mikidadi bin Ma'di Yakrib -Radhi za Allah ziwe juu yake- Kutoka kwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-: "Atakapompenda mtu ndugu yake basi na amueleze kuwa anampenda".
Imepokelewa na Abu Daud, Tirmidhiy na Nasai katika kitabu Alkubraa na AhmadAnabainisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- moja ya sababu ambazo hutia nguvu mahusiano kati ya waumini na hueneza mapenzi baina yao, nako ni kuwa mtu atakapompenda ndugu yake basi na amueleze kuwa anampenda.
Imepokewa kutoka kwa Abdillah Ibn Amri bin Aswi -Radhi za Allah ziwe juu yao wawili- kutoka kwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-amesema: "Madhambi makubwa: Ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na kuwaasi wazazi wawili, na kuuwa nafsi, na kiapo cha uongo".
Imepokelewa na Al-BukhaariyAnabainisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- madhambi makubwa, nayo ni yale aliyokemewa mfanyaji wake kwa kemeo la adhabu kali duniani au Akhera. La kwanza lake "Ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu": Nalo ni kukielekeza chochote katika aina za ibada kwa asiyekuwa Allah, na kumfanya kuwa sawa na Allah asiyekuwa Allah katika yale ambayo ni maalumu kwa Allah katika uungu wake na uumbaji wake na majina yake na sifa zake. Na la pili lake "Ni kuwaasi wazazi wawili": Nalo ni kila linalopelekea kuwaudhi wazazi wawili sawa sawa iwe kauli au kitendo, na kuacha kuwatendea wema. Na la tatu lake: "Ni kuua nafsi": Bila hatia, kama kuuwa kwa dhulma na uadui. Na la nne lake "Kiapo cha uongo": Nako ni kuapia uongo huku ukijua kuwa ni uongo, umeitwa hivyo; Kwa sababu humzamisha mfanyaji wake katika madhambi au motoni.
Kutoka kwa Abuu Huraira amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu -rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: "Mwenye kwenda upesi kuwasaidia wajane na maskini ni kama mwenye kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, au mwenye kusimama usiku na kufunga mchana"
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeAnaeleza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa mwenye kusimamia masilahi ya mwanamke aliyefiwa na mumewe na ikawa hakuna yeyote mwenye kusimamia mambo yake, na masikini muhitaji, na akawapa matumizi akitaraji malipo mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, basi mtu huyu katika malipo ni kama mpigana Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, na ni kama mwenye kusimama katika swala ya tahajudi asiyechoka, na mfungaji asiyefungua.
Imepokelewa Kutoka kwa Abuu Huraira -Radhi za Allah ziwe juu yake- kutoka kwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- amesema: "Yaepukeni mambo saba yenye kuangamiza" Wakasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ni yapi hayo? Akasema: "Ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu (na kitu kingine), na uchawi, na kuua nafsi aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa haki, na kula riba, na kula mali ya yatima, na kukimbia siku ya vita, na kuwatuhumu machafu waumini wa kike waliojihifadhi wasiojua lolote (kuhusu huo uchafu)"
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeAnaamrisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- umma wake kujitenga mbali na maovu saba na maasi yenye kuangamiza, na alipoulizwa ni yapi hayo? akayabainisha kuwa ni: La kwanza: Ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu kingine, kwa kujifanyia mshirika na mfano wake utakasifu ni wake kwa namna yoyote ile itakayokuwa, na kuielekeza aina yoyote ya ibada miongoni mwa ibada kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kaanza na ushirikina; kwa sababu ndio dhambi kubwa kuliko yote. La pili: Uchawi -Nao namna ya ufungaji mafundo na makombe na madawa na ufukishaji mioshi-, yanayoleta athari katika mwili wa mwenye kurogwa kwa kuua au kutia maradhi, au kuwatenganisha kati ya wana ndoa wawili, nayo ni kazi ya kishetani, na wengi wao hawaufikii uchawi isipokuwa kwa ushirikina na kujikurubisha kwa maruhani wachafu kwa kitu wanachokipenda. La tatu: Ni kuua nafsi aliyokataza Allah isiuliwe isipokuwa kwa kigezo cha kisheria, na hutekelezwa na hakimu. La nne: Kutumia riba kwa kula au kwa njia nyingine katika njia za kunufaika. La tano: Kufanya uadui katika mali ya mtoto mdogo aliyefiwa na baba yake naye akiwa chini ya umri wa kubalehe. La sita: Kukimbia katika vita kati ya waislamu na makafiri. La saba: Kuwatuhumu wanawake huru wenye kujizuia na machafu kwa uzinifu, na vile vile kuwatuhumu wanaume.