





























Hadeeth Cards
Da'wa cards that highlight great meanings from the noble prophetic hadiths in a simple style and attractive display that helps the Muslim to have a deeper understanding of his religion in an easy way
All
Kutoka kwa Sa'di radhi za Allah ziwe juu yake amesema: Alikuja bedui kwa Mtume -Rehema na Amani ziwe juu yake akasema: Nifundishe maneno nitakayoyasema. Akasema "Sema: Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu yeye pekee asiyekuwa na mshirika, Mwenyezi Mungu mkubwa mno, na kila sifa njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu kwa wingi, na ametakasika Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu, na hapana ujanja wala nguvu isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu mwenye nguvu na hekima" Akasema: Haya ni kwa ajili ya Mola wangu, yako wapi ya kwangu? Akasema: "Sema: "Ewe Mwenyezi Mungu nisamehe mimi na unihurumie na uniongoze na uniruzuku".
Imepokelewa Imamu MuslimMtu mmoja miongoni mwa watu wa kijijini alimuomba Mtume rehema na amani ziwe juu yake amfundishe dhikiri atakayokuwa akiisema, akasema rehema na amani ziwe juu yake: Sema: "Laa ilaaha illa llaah wahdahu laa shariika lahu" (Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, yeye pekee asiye na mshirika wake) Ameanza kwa shahada ya tauhidi, na maana yake hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, "Allaahu Akbaru kabiira" Yaani: Mwenyezi Mungu ni mkubwa kuliko kila kitu na ni Mtukufu, "Na Alhamdulillaahi kathira" Yaani: Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu kwa wingi, kwa sifa zake na vitendo vyake na neema zake zisizohesabika, "Sub-haanallaahi rabbil Aalamiin" Yaani: Ametukuka na kutakasika na kila mapungufu, "Laa haulaa walaa quwwata illaa billaahil Azizil Hakiim" Yaani: Hakuna namna ya kugeuka kutoka hali moja kwenda hali nyingine isipokuwa kwa uweza wa Allah na msaada wake na taufiki yake, Yule bwana akasema: Maneno haya ni kwa ajili ya Mola wangu Mlezi, kwa kumtaja yeye na kumtukuza, ya kwangu mimi ya kujiombea mwenyewe yako wapi? Mtume rehema na amani ziwe juu yake akasema kumwambia: Sema: "Ewe Mola wangu nisamehe" Kwa kuyafuta madhambi na kuyasitiri, "Na unihurumie" Kwa kuniletea manufaa na masilahi ya dini na dunia kwangu, "Na uniongoze" Kwenda katika hali nzuri na katika njia iliyonyooka, "Na uniruzuku" Mali ya halali na siha na kila aina ya kheri na afya.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Huraira -radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume -rehema na amani ziwe juu yake-: "Atakaye apa akasema katika kiapo chake: Na apa kwa Lata na uzza, basi aseme: Hapana apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na atakayesema kumwambia ndugu yake: Njoo tucheze kamari, basi na atoe sadaka".
Wamekubaliana Bukhari na Muslim juu ya usahihi wakeAnatahadharisha Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuapa kwa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu; kwani muumini haapi ila kwa Mwenyezi Mungu, Na anaeleza kuwa atakayeapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu; Kwa mfano mtu akiapa kwa Lata na Uzza - masanamu mawili yaliyokuwa yakiabudiwa katika zama za kabla ya Uislamu - basi aseme ndani ya nafsi yake: Hapana apasayekuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, ili ajiepushe na ushirikina na ili iwe ni fidia ya kiapo chake hicho. Kisha akaeleza rehema na amani ziwe juu yake kuwa atakayemwambia rafiki yake: Njoo tucheze kamari - ambayo ni watu wawili au zaidi watakaposhindana kwa sharti kuwa baina yao kuna pesa ambayo mshindi ataichukua, na kila mmoja wao lazima ima apate hasara au faida-; ni sunna atoe sadaka kwa kitu chochote kama kafara ya yale aliyoyahamasisha.
Imepokelewa kutoka kwa Abii Saidi Al-Khudry na kutoka kwa Abuu Huraira -Radhi za Allah ziwe juu yao- kutoka kwa Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- amesema: "Atanadi mwenye kunadi: "Hakika, mtapata afya nzuri na wala hamtougua milele. Na hakika, mtakuwa hai na wala hamtokufa milele, na hakika mtakuwa vijana na wala hamtazeeka milele. Na hakika, mtastareheka na wala hamtapata shida yoyote milele." Na hayo ndiyo kauli yake Mwenye Nguvu, Mtukufu: "Na wataitwa; (waambiwe) hiyo mbele yenu ndio pepo mliyorithishwa kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyafanya" [Al-Araf: 43].
Imepokelewa Imamu MuslimAmeeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa mwenye kunadi atanadi kuwaita watu wa peponi wakiwa humo wakineemeka: Hakika leo hii mtapata afya na hamtaugua peponi kamwe, kwa namna yoyote ile yatakavyokuwa madogo maradhi hayo, na hakika mtapewa uhai wala hamtakufa humo milele hata usingizi pia hamtaupata ambao ndio kifo kidogo, na leo mtaishi humo mkiwa vijana na wala hamtozeeka humo milele, nakuwa mtaneemeka humo wala hamtohuzunika milele, na hiyo ni kauli yake Mtukufu: "Na wataitwa (waambiwe) hiyo mbele yenu ndio pepo mliyorithishwa kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyafanya" [Al-Araf: 43].
Na imesimuliwa kutoka kwa Suhaib Mwenyezi Mungu amridhie, kutoka kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake amesema: "Wakati wakazi wa Peponi watakapoingia Peponi, Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kutukuka, atasema: "Je, mnataka kitu chochote niwazidishie?" Watasema: "Je, hukuziangaza nyuso zetu? Je, hukutuingiza Peponi, na ukatuokoa kutokana na Moto?" Kisha (Mwenyezi Mungu) atainua pazia, basi, hawatapewa kitu chochote kinachopendwa zaidi kwao kuliko kumwangalia Mola wao Mlezi Mwenye Nguvu, Mtukufu."
Imepokelewa Imamu MuslimAnaeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa watakapoingia watu wa peponi peponi, Mwenyezi Mungu aliyetakasika na kutukuka atasema kuwaambia: Je, mnahitaji chochote nikuongezeeni? Watasema watu wa peponi wote kwa pamoja: Kwani hujazitia nuru nyuso zetu, kwani hujatuingiza peponi, na ukatuokoa na moto? Hapo, Mwenyezi Mungu Mtukufu ataondoa pazia na kulinyanyua; na pazia lake ni nuru, watajikuta hawajapewa kitu wanachokipenda zaidi kwao kuliko kumtazama Mola wao Mlezi Aliyetakasika na kutukuka.
Imepokelewa kutoka kwa Jabiri -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- amesema: Nilimsikia Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- akisema: "Hakika shetani alishakata tamaa kuabudiwa na wenye kuswali katika kisiwa cha Arab, Lakini yuko katika kuwachochea baina yao".
Imepokelewa Imamu MuslimAmeeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa Ibilisi amekwishakata tamaa waumini wenye kuswali kurudi kuabudu na kusujudia masanamu katika kisiwa Arab, lakini bado anatamaa, na bado nguvu zake na juhudi zake na harakati zake ziko katika kuwachochea baina yao kwa ugomvi na chuki na vita na fitina na mfano wa hayo.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Huraira -Radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-: "Aina mbili za watu ni miongoni mwa watu wa motoni, sijawaona (katika zama zake Mtume), watu walio na mijeledi mithili ya mikia ya Ng'ombe wakiwapiga watu, na wanawake waliovaa na wako uchi, wanenguaji wakatikaji, vichwa vyao ni kama nundu za Ngamia zenye kuyumba (huku na kule), hawa, hawatoingia peponi, na wala hawatoipata harufu yake, na hakika harufu yake hupatikana umbali wa masafa kadhaa wa kadhaa".
Imepokelewa Imamu MuslimAnatahadharisha Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuhusu aina mbili za watu ambao ni katika watu wa motoni, hajawaona na hawakuwepo katika zama zake, bali aina hizo zitatokea baada yake: Aina ya kwanza: Ni watu walio na Mijeledi mirefu kama mikia ya Ng'ombe, wakiwapiga watu kwayo, nao ni Polisi na wasaidizi wa viongozi wasiowaadilifu, wanaowapiga watu bila hatia. Aina ya pili: Ni wanawake waliovua vazi la heshima na haya walizoumbiwa nazo mwanamke kawaida. Na sifa zao: Kwa muonekano wamevaa, na kwa uhalisia wako uchi; kwa sababu wamevaa nguo nyepesi zinazoonyesha ngozi, na wamefunika sehemu ndogo tu katika mili yao na wameacha wazi sehemu nyingine; kwa ajili ya kuonyesha urembo wao, nyoyo za wanaume zinavutika kwao kwa sababu ya mavazi yao, na kutembea kwao kwa maringo, wakinengua mabega yao, na wanawavutia wanawake wengine pia katika kupinda kimaadili, na kupotea waliko tumbukia ndani yake, Na miongoni mwa sifa zao pia: Vichwa vyao ni mfano wa nundu za Ngamia zilizopinda, utawakuta wakiipa kipaumbele mionekano ya vichwa vyao, wakiikuza kwa kukunja misuko na mfano wake, Na kufananishwa na nundu za Ngamia, ni kwa sababu kuinuka kwa nywele zao na misuko yao juu ya vichwa vyao, na kuzikunja kwao kwa sababu ya misuko mpaka zinalalia upande mmoja wa kichwa kama inavyolalia upande mmoja nundu ya Ngamia. Mwanamke atakayekuwa na sifa hizi, atakuwa na ahadi hii kali ya kutoingia peponi na wala hatopata harufu yake na wala hatoikaribia, na harufu ya pepo hupatikana na hunuswa kutoka masafa ya mbali.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Saidi Al-Khudri -Radhi za Allah ziwe juu yake- yakwamba Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- amesema: "Asiangalie mwanaume katika uchi wa mwanaume mwenzie, wala mwanamke kutazama uchi wa mwanamke mwenzie, na wala asijifunike mwanaume na mwanaume mwenzie shuka moja, na wala mwanamke asijifunike na mwanamke mwenzie shuka moja".
Imepokelewa Imamu MuslimAmekataza Mtume rehema na amani ziwe juu yake mwanaume kutazama uchi wa mwanaume mwenzie, au mwanamke kutazama uchi wa mwanamke mwenzie. Uchi: Ni kila kinachoonewa aibu kinapodhihiri, na uchi wa mwanaume ni kati ya kitovu chake na magoti yake, Na mwanamke mwili wake wote ni uchi kwa mwanamke asiye mume wake au ndugu wa damu, na upande wa wanawake kwa ndugu zao wa damu, anaweza kuonyesha viungo ambavyo kwa desturi ya kawaida huonekana wakati wa kufanya kazi zake za nyumbani. Na amekataza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kukaa faragha mwanaume na mwanaume mwenzake ndani ya nguo moja, au ndani ya kifuniko kimoja wakiwa uchi, na mwanamke kukaa faragha na mwanamke mwenzie ndani ya nguo moja au ndani ya kifuniko kimoja wakiwa uchi; kwa sababu kitendo hicho huenda kikapelekea kila mmoja kugusa uchi wa mwenzie, na kuugusa ni haramu ni kama kuuangalia, bali hilo ni haramu zaidi; kwa sababu linapelekea katika uovu mkubwa.
Imepokelewa kutoka kwa Anas -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe ju yake- amesema: Alikuja mtu mmoja kwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi sijaacha dhambi yoyote wala maasi yoyote isipokuwa nimeyafanya, akasema: "Hivi wewe hautamki neno la shahada "Ash-hadu an-laa ilaaha illa llahu wa anna Muhamadan rasuulullah?" Akarudia mara tatu. Akasema: Ndiyo, akasema: "Kwa hakika tamko hilo hufuta makosa hayo yote."
Imepokelewa na Abu Yaala, Twabarani na Dhwiyau AlmaqidisiAlikuja mtu mmoja kwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-akasema: @Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi sijaacha dhambi yoyote wala maasi yoyote madogo wala makubwa isipokuwa nimeyafanya, je mimi nitakuwa ni mwenye kusamehewa? Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- akasema kumwambia: Hivi wewe hautamki neno la shahada "Ash-hadu an-laa ilaha illa llahu wa anna Muhamadan rasuulullah? Akarudia kumwambia hivyo mara tatu, Basi akajibu: Ndiyo nashuhudia, Basi Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- akampa habari ya ubora na utukufu wa shahada mbili na namna inavyofuta makosa, na kuwa toba hufuta makosa yaliyopita.
Imepokelewa kutoka kwa Jaabir -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao- kuwa Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- amesema: "Msijifunze elimu kwa ajili ya kujifaharisha kuwa ni katika maulama, wala kwa kujadiliana na wasiokuwa na elimu, wala kuonekana ni mtu bora kwenye vikao, na yeyote atakaye fanya hivyo basi anastahiki kuingia motoni."
Imepokelewa na Ibnu MaajahAmetahadharisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kutafuta elimu kwa lengo la kujifaharisha kuwa naye ni katika Maulamaa, na kujitangaza kuwa mimi ni mjuzi kama nyinyi, au kwa ajili ya kujadiliana na wasiokuwa na ujuzi katika dini wenye upungufu wa maarifa, au anajifunza ili aonekane kuwa mtu bora kwenye vikao na kupewa kipaumbele kuliko mtu mwingine, Basi yeyote atakaye fanya hivyo; Bila shaka anastahiki kuchomwa katika moto kwa sababu ya kujionesha kwake na kukosa Ikhlaas katika kuitafuta elimu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.