





























Hadeeth Cards
Da'wa cards that highlight great meanings from the noble prophetic hadiths in a simple style and attractive display that helps the Muslim to have a deeper understanding of his religion in an easy way
All
Kutoka kwa mama wa waumini mama Abdillah Aisha radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, amesema: Amesema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: "Yeyote atakayezua (kitu) katika jambo letu hili (dini) ambalo si miongoni mwake, basi hilo litakataliwa." Na katika riwaya nyingine ya Imamu Muslim: "Atakayefanya amali yoyote isiyokuwa na amri yetu basi itakataliwa".
Imepokelewa na Bukhari na MuslimAnabainisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa atakayetunga au kubuni jambo katika dini au akafanya amali yoyote ambayo haikuelekezwa na dalili yoyote kutoka katika Qur'ani na Sunna, basi jambo hilo litarejeshwa kwa mfanyaji wake na halitokubaliwa mbele ya Allah.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Huraira Abdul-Rahman bin Swakhar -radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Nilimsikia Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- akisema: "Yale niliyokukatazeni basi yaepukeni, na yale niliyokuamrisheni basi fanyeni katika hayo kadiri muwezavyo, na hakika waliangamia wale waliokuwa kabla yenu, kwa kukithiri maswali yao, na kuhitilafiana kwao na Manabii wao".
Imepokelewa na Bukhari na MuslimAmetubainishia sisi Mtume rehema na amani ziwe juu yake ya kuwa atakapotukataza kitu basi ni wajibu juu yetu kukiacha pasina kubagua, na atakapotuamrisha kwa chochote basi ni juu yetu kukifanya kile tunachokiweza. Kisha akatutahadharisha ili tusije kuwa kama baadhi ya umma zilizopita pindi walipokithirisha maswali juu ya Manabii wao ikiwa ni pamoja na kwenda kinyume nao, basi Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa aina mbali mbali za maangamivu na uharibifu, tunatakiwa tusiwe mfano wao ili tusiangamie kama walivyoangamia.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Huraira -radhi za Allah ziwe juu yake- amesema: Amesema Mtume -rehema na amani ziwe juu yake-: "Hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri hakubali ila vizuri, na hakika Mwenyezi Mungu amewaamrisha waumini kwa yale aliyowaamrisha kwayo Manabii, akasema Allah Mtukufu: "Enyi Mitume! Kuleni katika vile vilivyo vizuri na mtende mema, hakika mimi kwa yale mnayoyafanya ni Mjuzi" [Al-Muuminuun: 51] Na akasema Allah Mtukufu: "Enyi mlioamini! Kuleni katika vizuri miongoni mwa vile tulivyokuruzukuni, na mumshukuru Mwenyezi Mungu ikiwa kweli nyinyi mnamuabudu yeye peke yake" [Al-baqara: 172] akasema: Kisha akataja tukio la mtu mmoja mwenye safari ndefu, nywele zake zimetimka, kajaa vumbi, ananyanyua mikono yake kuelekea mbinguni (anasema) Mola wangu Mola wangu! (wakati huo) chakula chake ni cha haramu, na mavazi yake ni ya haramu, na kinywaji chake ni cha haramu, na lishe yake yote ni ya haramu, itawezekana vipi kujibiwa kwa mtu kama huyo?!".
Imepokelewa Imamu MuslimAlieleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa Mwenyezi Mungu ni mzuri na ni mtakasifu ametakasika na kila mapungufu na aibu na amesifika kwa yote yaliyokamilika, na wala hakubali katika matendo kauli na itikadi isipokuwa ile itakayokuwa nzuri, nayo ni ile iliyotakaswa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, yenye kwenda sambamba na muongozo wa Mtume rehema na amani ziwe juu yake, na haitakiwi mtu ajikurubishe kwa Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa hayo, na katika mambo yanayosababisha amali kuwa nzuri kwa muumini ni chakula chake kuwa kizuri, na kiwe kimetokana na halali, kwa hilo amali zake zinakuwa njema, na ndio maana Mwenyezi Mungu aliwaamrisha waumini kwa lile alilowaamrisha Mitume, ikiwemo kula halali na kutenda mema, akasema: "Enyi Mitume! Kuleni katika vilivyo vizuri na mtende mema, hakika mimi kwa yale mnayoyafanya ni Mjuzi" Na akasema: "Enyi mlioamini kuleni katika vizuri katika vile tulivyokuruzukuni". Kisha akatahadharisha rehema na amani ziwe juu yake kula haramu,ambako kunaharibu matendo na kunazuia kukubalika kwake kwa sababu yoyote ile inayoonekana; ikiwemo: Ya kwanza: Kuwa na safari ndefu iliyo katika misingi ya kumtii Mwenyezi Mungu kama Hija na Jihadi na kuunga udugu na mengineyo. Ya pili: Nywele kukaa hovyo kwa kutotanwa, na kubadilika rangi ya ngozi na rangi ya nguo kwa sababu ya udongo, basi mtu huyu anakuwa kadharurika. Ya tatu: Ananyanyua mikono yake juu mbinguni kwa dua. Ya nne: Anamuomba Mwenyezi Mungu kupitia majina yake na anang'ang'ania katika hilo: Ewe Mola wangu Ewe Mola wangu! Na pamoja na sababu hizi za kujibiwa dua hakusikilizwa; na hii ni kwa sababu chakula chake na kinywaji chake na mavazi yake ni vya haramu, na afya yake imetokana na haramu, ni mbali sana kwa mtu mwenye sifa kama hizi kujibiwa, na atajibiwa vipi?!
Kutoka kwa Abul-Abbas, Abdallah bin Abbas radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao amesema: Siku moja nilikuwa nyuma ya Mtume rehema na amani ziwe juu yake akasema: "Ewe kijana, hakika mimi ninakufundisha maneno: Muhifadhi Mwenyezi Mungu naye atakuhifadhi, muhifadhi Mwenyezi Mungu utamkuta uendako, utakapo omba basi muombe Mwenyezi Mungu, na ukitaka msaada muombe msaada Mwenyezi Mungu, na tambua: kuwa laiti watu wote wangelikusanyika ili wakunufaishe wewe kwa kitu chochote, hawatoweza kukunufaisha isipokuwa kwa kitu ambacho tayari kakiandika Mwenyezi Mungu kwako, na ikiwa watakusanyika kwa ajili ya kukudhuru wewe kwa kitu chochote, hawatoweza kukudhuru kwa kitu chochote isipokuwa kile ambacho kakuandikia Mwenyezi Mungu kikupate, kalamu zimenyanyuliwa na kurasa zimekauka" Na katika riwaya isiyokuwa ya Tirmidhi: "Muhifadhi Mwenyezi Mungu utamkuta mbele yako, Jipendekeze kwa Mwenyezi Mungu wakati wa raha atakujua wakati wa shida, na tambua kuwa yaliyo kukosa hayakua ni yenye kukupata, na yaliyo kupata hayakuwa ni yenye kukukosa, na tambua kuwa msada huambatana na subira, na kuwa faraja huwa pamoja na matatizo, na kuwa uzito huwa pamoja na wepesi".
Imepokelewa naTirmidhiy na wengineoAnaeleza bin Abbas -radhi za Allah ziwe juu yake- kuwa yeye alipokuwa kijana mdogo alikuwa kapanda pamoja na Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-, akasema kumwambia -Amani iwe juu yake-: Hakika mimi ninakufundisha vitu na mambo ambayo Mwenyezi Mungu atakunufaisha kwayo: Muhifadhi Mwenyezi Mungu kwa kuhifadhi maamrisho yake na kuepuka makatazo yake, kiasi kwamba akukute katika utiifu na yale yenye kukuweka karibu naye, na asikukute katika maasi na madhambi, ikiwa utafanya hivyo basi malipo yako yatakuwa ni Mwenyezi Mungu kukuhifadhi kutokana na kero za Dunia na Akhera, na atakunusuru katika mambo yako magumu mahala popote utakapoelekea. Na ukitaka kuomba jambo, basi usimuombe ila Mwenyezi Mungu kwani Yeye pekee ndiye mwenye kuwajibu waombaji. Na ukitaka msaada basi usiutake ila kwa Mwenyezi Mungu. Na uwe na yakini kuwa hutopata manufaa yoyote hata kama viumbe wote wa Ardhini watakusanyika ili kutaka kukunufaisha, isipokuwa kwa kile alichokiandika Mwenyezi Mungu kwako, na wala hutopata madhara hata kama viumbe wote wa Ardhini watakusanyika ili kutaka kukudhuru, isipokuwa kwa lile alilolikadiria Mwenyezi Mungu juu yako. Na kuwa jambo hili kashaliandika Mwenyezi Mungu Mtukufu na akalikadiria kulingana na namna hekima na elimu yake zilivyopelekea, na hakuna kubadilishwa yale aliyoyaandika Mwenyezi Mungu. Na kwamba atakayemuhifadhi Mwenyezi Mungu kwa kuhifadhi amri zake na kuyaepuka makatazo yake; basi Mwenyezi Mungu Mtukufu atakuwa mbele ya mja kwa kuyajua matatizo yatakayomfika na atamnusuru na kumpa msaada. Na kwamba mwanadamu atakapomtii Mwenyezi Mungu wakati wa raha basi Mwenyezi Mungu atamletea faraja na njia ya kutokea wakati wa shida, hivyo na aridhie kila mja na kile alichokikadiria Mwenyezi Mungu cha kheri na shari. Na kukiwa na matatizo na mitihani basi mja ashikamane na subira kwani subira ni ufunguo wa faraja, na kwamba mitihani ikizidi kuwa mingi ndio faraja huja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na kwamba uzito unapotokea Mwenyezi Mungu huufuatisha na wepesi.
Kutoka kwa Abuu Amri - na inasemekana ni Abuu Amra, Sufiani bin Abdillah radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema: Nilisema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Nieleze ndani ya Uislamu kauli ambayo sitomuuliza yeyote zaidi yako, akasema: "Sema: Nimemuamini Mwenyezi Mungu, kisha kuwa na msimamo".
Imepokelewa Imamu MuslimSwahaba Sufiani bin Abdillah radhi za Allah ziwe juu yake alimuomba Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- amfundishe kauli iliyokusanya maana nzima ya Uislamu ili ashikamane nayo na wala hatomuuliza yeyote zaidi yake? Akasema Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake-: Sema: Nimempwekesha Mwenyezi Mungu, na nimemuamini kuwa yeye ndiye Mola wangu na Mungu wangu na Muumba wangu na muabudiwa wangu wa haki aisye na mshirika wake, kisha awe mtiifu katika sheria za Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza faradhi za Mwenyezi Mungu na kuacha maharamisho ya Mwenyezi Mungu na adumu katika hilo.
Kutoka kwa Abuu Abdillaah Jabiri bin Abdillah Al-Aswari radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao: Kuwa mtu mmoja alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu -rehema na amani ziwe juu yake-akasema: "Waonaje ikiwa nitaswali swala zilizofaradhishwa, na nikafunga Ramadhani, na nikahalalisha kilichokuwa halali na nikaharamisha kilichokuwa haramu, na wala sikuzidisha zaidi ya hayo je nitaingia peponi?Akasema: "Ndiyo".
Imepokelewa Imamu MuslimAnaweka wazi Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake kuwa yeyote atakayeswali swala tano zilizofaradhishwa na wala hakuzidisha zaidi ya hizo swala tano kwa kuswali swala za Sunna, na akafunga mwezi mtukufu wa Ramadhani na akawacha kufunga funga za sunna, na akaamini uhalali wa vilivyo halali na akavitekeleza na akaamini uharamu wa vilivyo haramu na akajiepusha navyo, kwa hakika mtu huyo ataingia Peponi.
Kutoka kwa Muadhi bin Jabali radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema: Nilisema ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hebu nieleze amali itakayoniingiza peponi na kuniweka mbali na Moto, akasema: "Hakika umeniuliza kuhusu jambo kubwa, lakini nijepesi kwa yule atakayefanyiwa wepesi na Mwenyezi Mungu: Ni kumuabudu Mwenyezi Mungu bila kumshirikisha na chochote, na kusimamisha swala, na kutoa zaka, na kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, na kuhiji. kisha akasema Mtume: Je, nikujulishe milango ya kheri? Funga ni kinga, na sadaka inaondosha madhambi kama maji yanavyo uzima moto, na swala ya mtu katikati ya usiku, kisha akasoma kauli ya Mwenyezi Mungu: "Mbavu zao zinaachana na vitanda..." mpaka alipofikia mwisho wa aya "wanayoyatenda". Kisha akasema Mtume: Je nikueleze kichwa cha mambo yote na nguzo yake na kilele chake? Nikajibu ndio ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu, akasema: kichwa cha mambo yote ni Uislamu, na nguzo yake ni Swala, na kilele chake ni Jihadi. Kisha akasema: Je nikujulishe kinachoyahifadhi na kuyatunza matendo hayo? Nikasema ndio ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, akaushika ulimi wake kisha akasema: Zuia ulimi wako, nikamuuliza: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu je tutahesabiwa kwa kila tunacho kizungumza? Akasema: Akukose mama yako, hakuna kitakacho waingiza watu wengi motoni kama maneno wanayoyazungumza."!
Imepokelewa Imamu TirmidhiyAmesema Muadhi radhi za Allah ziwe juu yake: Tulikuwa pamoja na Mtume rehema na amani ziwe juu yake katika safari, siku moja nikawa karibu naye tukiwa tunatembea, nikasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu nieleze amali itakayoniingiza Peponi na kuniweka mbali na moto, akasema: Bila shaka umeuliza kuhusu jambo kubwa kulifanya kwake katika nafsi, na bila shaka ni jepesi na ni rahisi mno kwa atakayerahisishiwa na Mwenyezi Mungu kulifanya; tekeleza faradhi za Uislamu; Ya kwanza: Umuabudu Mwenyezi Mungu peke yake na wala usimshirikishe na chochote. Ya pili: Usimamishe swala tano za faradhi mchana na usiku: Alfajiri, Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, Ishaa, kwa sharti zake na nguzo zake na wajibu wake. Ya tatu: Utoe zaka ya wajibu, nayo ni ibada ya mali ya wajibu kwa kila mali iliyofikia kiwango katika sheria, na wanapewa wastahiki wake. Ya nne: Ufunge mwezi wa Ramadhani, nako ni kujizuia na kula na kunywa na mengineyo katika mambo yenye kufunguza kwa nia ya kumuabudu Mwenyezi Mungu, kuanzia kuchomoza kwa Alfajiri mpaka kuzama kwa Jua. Ya tano: Utaizuru nyumba kwa kwenda Makka ili kutimiza ibada, kwa lengo la kumuabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kisha akasema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: Je nikufahamishe kuhusu njia inayokufikisha katika milango ya heri? Nayo ni kwa kutekeleza faradhi na sunna hizo: Ya kwanza: Ni funga ya hiyari, nayo inamzuia mtu kuingia katika maasi, nayo ni kwa kuvunjavunja matamanio, na kuzidhoofisha nguvu. Ya pili: Sadaka ya kujitolea inazima madhambi baada ya kuyafanya na huyaondosha na kufuta athari zake. Ya tatu: Swala ya tahajudi katika theluthi ya mwisho ya usiku, kisha akasoma rehema na amani ziwe juu yake kauli yake Mtukufu: "Hunyanyuka mbavu zao" Yaani: Hujiweka mbali, na "malazi" Yaani: Mahali pa kulala, "wakimuomba Mola wao Mlezi" Yaani: kwa swala na dhikri na kusoma Qur'ani na dua, "kwa hofu na tamaa, na katika yale tuliyowaruzuku wanatoa, hakuna nafsi ijuayo yale waliyofichiwa, katika yale yenye kutuliza macho" Yaani: Yale yenye kutuliza macho yao siku ya Kiyama na katika pepo miongoni mwa neema, "ni malipo kwa yale waliyokuwa wakiyafanya". Kisha akasema rehema na amani ziwe juu yake: Hivi nikueleze msingi wa dini? na nguzo yake inayosimamia? na kiini cha kilele chake? Akasema Muadhi radhi za Allah ziwe juu yake: Ndio, nieleze ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Akasema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: Kichwa cha mambo yote ni: Uislamu nao ni shahada mbili, na kwa shahada hizi mbili ndio mtu anapata msingi wa dini. Na nguzo yake: Ni swala, hakuna Uislamu bila swala, kama ambavyo nyumba haiwezi kusimama pasina nguzo, atakaye swali dini yake itakuwa na nguvu na itanyanyuka; Na kiini cha kilele chake na kimo chake ni Jihadi na kutoa juhudi katika kupambana na maadui wa dini ili kulinyanyua neno la Mwenyezi Mungu. Kisha akasema rehema na amani ziwe juu yake: Hivi nikuelezeni umadhubuti na ufanisi wa yaliyopita? Mtume rehema na amani ziwe juu yake akashika ulimi, na akasema: Zuia huu na wala usizungumze yale yasiyokuhusu. Akasema Muadhi: Je atatuchukulia makosa na kutuhesabu Mola wetu Mlezi na kutuadhibu kwa kila tunachozungumza?! Akasema rehema na amani ziwe juu yake: Amekupoteza mama yako! Na makusudio yake si kumuombea dua mbaya, bali ni katika maneno ya waarabu yaliyokuwa yakitumika kumtanabahisha mtu kuwa jambo hili unatakiwa kulichukulia tahadhari kubwa na kulielewa, kisha akasema; na unadhani ni kipi kitawatupa watu na kuwadondosha kwa nyuso zao ndani ya moto zaidi ya chumo za ndimi zao, ikiwemo ukafiri na kumzulia mtu machafu na matusi na utesi na usengenyaji, na uongo na mfano wa hayo.
Kutoka kwa bin Abbas radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake kutoka kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake katika yale anayoyapokea kutoka kwa Mola wake Mlezi Aliyetukuka amesema: "Hakika Mwenyezi Mungu aliandika mema na maovu, kisha akalibainisha hilo, basi yeyote atakayepania jema akawa hakulifanya; Mwenyezi Mungu huliandika kwake kuwa ni jema kamili, na akilipania na akalifanya; basi Mwenyezi Mungu huliandika kwake kuwa ni mema kumi mpaka ziada mia saba mpaka nyongeza nyingi zaidi, na akipania baya akawa hakulifanya; Mwenyezi Mungu huliandika kwake kuwa ni jema moja kamili, na akikusudia na akalifanya; basi Mwenyezi Mungu huliandika kuwa ni ovu moja".
Imepokelewa na Bukhari na Muslim katika sahihi zao kwa herufi hiziAnabainisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- yakuwa Mwenyezi Mungu amepanga mema na maovu, kisha akawabainishia Malaika wawili ni namna gani watayaandika: Atakayetaka na akakusudia na akaazimia kufanya jema basi litaandikwa kwake jema moja, hata kama hatolifanya, na ikiwa atalifanya basi hulipwa mara dufu kwa mara kumi mfano wake, mpaka ziada ya mia saba, mpaka ziada nyingi zaidi, na ziada huendana na yale yaliyoko moyoni kwanzia Ikhlaswi (kutakasa nia) na kuwanufaisha wengine, n.k. Na atakayetaka na akakusudia na akaazimia kufanya uovu kisha akauacha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, huanidikiwa jema moja, na ikiwa atauacha kwa sababu ya kukosa muda wa kuufanya na akiwa hajafanya sababu za kuuendea, hatoandikiwa chochote, na akiuacha kwa kushindwa huandikwa nia yake pekee, na ikiwa ataufanya litaandikwa kwa ovu moja.
Kutoka kwa Abuu Huraira radhi za Allah ziwe juu yake amesema: Amesema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: "Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: Atakayemfanyia uadui kipenzi changu basi hakika nimemtangazia vita, na hatojiweka karibu kwangu mja wangu kwa kitu ninachokipenda zaidi kuliko kile nilichomfaradhishia, na hatoacha mja wangu kuendelea kujiweka karibu yangu kwa mambo ya sunna mpaka nitampenda, nikishampenda nitakuwa sikio lake analosikilizia, na jicho lake analoonea, na mkono wake anaokamatia, na mguu wake anaotembelea, na akiniomba hakika nitampa, na akinitaka ulinzi hakika nitamlinda".
Imepokelewa na Al-BukhaariyAmeeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake katika hadithil-Qudsi ya kwamba Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kutukuka alisema: Atakayemuudhi kipenzi miongoni mwa vipenzi vyangu na akamkasirisha na akamchukiza basi nitakua nimemjulisha na nimemtangazia uadui. Walii (Kipenzi): Ni muumini mchamungu, na kwa kadiri itakavyokuwa imani na uchamungu kwa mja ndivyo inavyokuwa nafasi yake ya kupendwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hajawahi kujiweka karibu Muislamu kwa jambo analolipenda zaidi Mwenyezi Mungu kuliko lile alilomfaradhishia na kumuwajibishia kama kufanya ibada na kuacha maharamisho, na hatoacha Muislamu kujiweka karibu kwa Mola wake Mlezi kwa ibada za sunna pamoja na faradhi mpaka atayapata mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu akimpenda basi yeye huwa msimamizi wake katika viungo hivi vinne: Anamsimamia katika masikio yake, hayatosikia ila yale yanayomridhisha Mwenyezi Mungu. Na anamsimamia katika macho yake, hatotazama ila yale anayoyapenda Mwenyezi Mungu kuyatazama na kuyaridhia. Na anamsimamia katika mkono wake, hatofanya kwa mkono wake ila yale yanayomridhisha Mwenyezi Mungu. Na atamsimamia katika mguu wake, hatokwenda ila katika yale yanayomridhisha Mwenyezi Mungu, na hatokwenda mbio ila katika yale yenye kheri. Na pamoja na hayo, akimuomba Mwenyezi Mungu chochote basi Mwenyezi Mungu atampa alichoomba, anakuwa ni mtu mwenye kujibiwa dua, na akitaka ulinzi kwa Mwenyezi Mungu na akaomba hifadhi kwake kwa kutaka alindwe, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu atamlinda na kumhami na yale anayoyaogopa.